Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Zuchu amesema katika moja ya mafanikio ambayo hakuwahi kuyadhania awali ni kutengeneza fedha katika mitandao ya kijamii kupitia sanaa yake ya muziki.

Zuchu ameyasema hayo visiwani Unguja wakati wa mafunzo maalum kwa wasanii yaliyolenga kukuza vipaji vyao, pamoja na kutumia sanaa zao kujinufaisha kibiashara.

Akitolea mfano amesema kwa mara ya kwanza anapigiwa simu kwamba amewekewa kiasi cha fedha ‘Euro 4,000’ hakudhani kama ipo siku angetengeneza fedha mitandaoni.

“Kipindi natoa Zuchu Ep nikapigiwa simu hela yangu ya youtube imeingia, kipindi hicho nilikuwa sijui sana mambo ya Euro inachenjiwa vipi, niliambiwa nimewekewa euro 4,000 kwenye akaunti yangu kupitia akaunti ya youtube nikasema aaah hizo zitakuwa ni hela ndogo tu…

“Hapo nimetoka kupewa hela ya nauli Sh20,000 na bosi sijaanza kukamata hela, siku moja nikasema ngoja nipite benki, nikauliza euro 4,000 ni shilingi ngapi nikaambiwa ni kama Sh10 milioni nilishangaa sana. Nikaanza kupiga simu mara mbili mbili hiyo ni pesa yangu ya mwezi mmoja siamini, hivyo msishangae ukiona mtu anashangilia kupata watazamaji milioni moja YouTube ujue anashangilia pesa,” amesema Zuchu.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Waziri wa Sanaa visiwani humo na kuendeshwa na jopo la wataalamu mbalimbali wa sanaa ya muziki kupitia tamasha la ‘Zuchu Home Coming’ linalotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *