Klabu ya Yanga kesho itashuka dimbani kupambana na Mtibwa Sugar kwenye mechi ya ligi kuu Tanzania Bara itakayofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Yanga wametambulisha Uwanja wa Uhuru kama uwanja wa nyumbani kwa sasa baada ya kupeleka maombi Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF) ambako baada ya kuyafanyiwa tathimini kwa mujibu kanuni hiyo ya sita, kipengele cha sita, TFF imeiridhia klabu hiyo kutumia uwanja wa Uhuru.
Hatua hiyo inafuatia baada ya Serikali ambaye ndiye mmiliki wa viwanja vya Uhuru na Uwanja Mkuu wa Taifa, kuzuia klabu hiyo pamoja na ya Simba kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa michezo yao ya nyumbani kutokana na vurugu.
Michezo mingine itakayopigwa Jumatano ni kati ya Mbeya City na Simba, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya; Majimaji itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea wakati JKT Ruvu itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Stand United itaikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na katika mkoa huo huo Mwadui itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye dimba la Mwadui Complex huku timu pinzani za Mwanza kati ya Mbao na Toto Africans itapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo.