Yanga leo inashuka dimbani dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara utakaofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilitakiwa kuchezwa mwanzoni mwa msimu, lakini ilishindwa kufanya hivyo baada ya kusogezwa mbele kutokana na kukabiliwa na michuano ya kimataifa.
Yanga leo itacheza bila Kocha wake Mkuu, Hans Pluijm aliyejiuzulu nafasi yake na sasa taarifa kutoka Yanga zinaeleza kuwa kikosi kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Juma Mwambusi na Meneja Hafidh Salehe hadi uongozi wa timu hiyo utakapoamua hatma yao.
Kocha huyo amejiuzulu baada kuwepo kwa taarifa za ujio wa Kocha mpya Mzambia wa Zesco, George Lwandamina aliyekuwepo jijini Dar es Salaam kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Yusuf Manji kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Pluijm.
Huo ni mchezo muhimu kwa Yanga kushinda ili kuzidi kujitengenezea mazingira ya kuwa karibu na wapinzani wao Simba ambao wamewaacha kwa tofauti ya pointi nane.
Yanga imeshacheza michezo 10, imeshinda sita, imepata sare tatu, na kupoteza moja ikivuna pointi 21 na JKT Ruvu imecheza michezo 11, imeshinda moja, ina sare sita na kupoteza minne ikishika nafasi ya pili kutoka mwisho kwa pointi tisa.