Mshauri maalumu wa Rais wa Gambia Adama Barrow amesema zaidi ya dola za Kimarekani milioni 11 zinaaminika kutoweka katika hazina ya serikali, kufuatia kuondoka madarakani Yahya Jammeh.
Mia Ahmad Fatty amewaambia Waandishi wa habari katika mji mkuu wa Senegal Dakar kwamba wataalamu wa masuala ya fedha wanatathmini kujua ni kiasi gani kwa sasa kimepotea.
Amesema Gambia kwa sasa ina tatizo kubwa kifedha kwa hazina yake kutokuwa na kitu kabisa baada ya kuondoka rais huyo.
Kwa sasa Rais Barrow amekuwa akifanya kazi na timu ya wataalamu wa masuala ya fedha na wengine kutoka Benki kuu ya nchi hiyo kupata kiasi halisi kilichopo.
Habari zinasema magari ya kifahari na mali nyingine zilionekana zikipakiwa katika ndege ya mizigo ya Chad kwa niaba ya Rais Jammeh siku alipoondoka nchini humo.
Maelfu ya watu walikusanyika katika Ikulu ya nchi hiyo jana jioni wakiyaangalia majeshi ya Senegal yakiingia kwa ajili ya kuweka usalama kabla ya kurejea nchini kwa Adama Barrow.