Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco imefanikiwa kutwaa ubingwa wa klabu bingwa Afrika baada ya kuifunga Al Ahly 1-0 kwenye mechi ya pili ya fainali iliyofanyika nchini Morocco.
Bao la ushindi la Wydad Casablanca lilifungwa na El Karti kipindi cha pili na kufanya matokeo ya jumla katika mechi zote mbili kuwa 2-1, baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 wiki mbili zilizopita nchini Misri.
Ubingwa huo kwa Wydad unakuwa wa pili tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo ambapo mara ya kwanza kutwaa ilikuwa ni mwaka 1992.
Wydad sasa itaiwakilisha Afrika kwenye michuano ya kombe la dunia la vilabu mwezi Desemba mwaka huu.
Michuano hiyo itafanyika katika nchi za falme za kiarabu (UAE) ambapo wataungana na timu nyingine kutoka kwenye mabara mengine ikiwemo mabingwa wa Ulaya klabu ya Real Madrid.