Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na vyuo vikuu.
Badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato cha sita.
Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.
Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.
Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
Naibu Waziri huyo amesema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.