Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali imekwishaipatia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba iliyokuwa inazikabili hospitali mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Manyara aliposimama wilayani Babati akiwa njiani kwenda Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku saba inayotarajiwa kuanza kesho.
Amesema suala la dawa kwa sasa linaenda vizuri, hivyo amewataka viongozi wa mikoa kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyopelekwa katika hospitali zao zinatumika kama ilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kuweka utaratibu wa kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa pamoja na kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuwawezesha kupata huduma ya matibabu bure kwa mwaka mzima.