Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema inatambua na itaendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wasio na uwezo wa kugharimia huduma za matibabu wanapatiwa msamaha wa matibabu katika ngazi zote kuanzia zahanati, vituo vya afya, hospitali za mikoa na za rufaa.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyasema hayo katika tamko lake kuhusu huduma za matibabu kwa walemavu wasio na uwezo na kusema hatua hiyo itawaondolea vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu wenye ulemavu katika kuzifikia huduma za afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.
Amesema kutokana na maelezo hayo, Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inatambua kuwa wapo wananchi wanakabiliwa na matatizo mbalimbali katika kuzifikia huduma za afya wakiwemo watu wenye ulemavu.
Ummy amesema kuwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010, pamoja na mambo mengine, inabainisha kuwa watu wenye ulemavu wana haki ya kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za afya.
Pia amesema serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha makundi maalumu wakiwemo watu wenye ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma za matibabu wanapata msamaha wa matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Amesema mtumishi atakayethibitika kuonesha kwenda kinyume cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za afya kwa kufanya vitendo vya unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi maalumu ikiwemo watu wenye ulemavu atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.