Wimbo wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Anjella uitwao ‘Kioo’ aliomshirikisha Bosi wake Harmonize umeondolewa kutoka kwenye mtandao wa Youtube kutokana na malalamiko ya hakimiliki kutoka Kampuni ya Mr Eazi ya Empawa Africa.
Hayo yanajiri baada ya Januari 2020 video ya wimbo wa msanii kutoka Konde Gang, Killy unaokwenda kwa jina la Ni Wewe ambao amemshirikisha Harmoninze nao kuondolewa YouTube kutokana na malalamiko ya hakimiliki kutoka kwa mtu anayetambulika kwa jina la Mutisya Munyithya kutoka Kenya.
Juni 2021, Wimbo wa Harmonize wa Sandakalawe nao uliondolewa YouTube kutokana na masuala ya hakimiliki baada ya kampuni ya usambazaji muziki ya Empire kulalamika kuwa wimbo huo umechukua baadhi ya vionjo kutoka kwao.
Kabla ya hapo, Agosti 2020, wimbo mwingine wa Harmonize wa Ameen uliondolewa YouTube baada ya rapa Rosa Ree kulalamika ulitumia mdundo wa wimbo wake wa Kanyor Aleng bila idhini yake hivyo alikiuka taratibu za hakimiliki.
Huo ulikuwa ni wimbo wa pili kwa Harmonize kuondolewa YouTube kutokana na mdundo wake kuonekana kunakiliwa kutoka kwenye wimbo mwingine. Wa kwanza ni Uno ambao prodyuza wa Kenya, Magix Enga alipeleka malalamiko yake kwenye mtandao huo kisha wakauondosha kwa muda.