Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema Wilaya hiyo imetenga maeneo saba likiwemo viwanja vya Biafra vilivyopo Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kwa ajili ya wamachinga ambao hawana maeneo ya kufanyia biashara zao.

Hapi amesema eneo hilo litakuwa likifanyiwa biashara siku ya Jumamosi na kwamba maeneo mengine yamepangiwa siku maalumu ambapo wamachinga watakuwa wanakwenda kufanya biashara.

Maeneo mengine ni Kata ya Bunju katika Soko la Matunda ambako biashara zitafanywa siku ya Jumatano, Kijitonyama soko litaanzia kwenye mataa hadi stendi ya zamani siku ya Jumanne huku Kata ya Msasani, gulio litafanyika katika Soko la Magunia siku ya Jumapili.

Amesisitiza kuwa lengo la kugawa maeneo hayo ni kuwasaidia wafanyabiashara ndogondogo kwenda kufanya biashara katika maeneo yaliyopangwa kulingana na siku yake.

Mkuu wa wilaya ameongeza kuwa miundombinu mbalimbali katika maeneo yaliyotengwa yanaendelea kurekebishwa ikiwemo ujenzi wa vyoo vya kuhama.

Hapi amesema manispaa hiyo haina wafanyabiashara wengi isipokuwa maeneo ya Tegeta na Bunju ambako ndio kuna changamoto ya wafanyabiashara wadogo wadogo.

Pia amesema wafanyabiashara ambao hawatafuata agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria na kuwataka wazingatie usafi ili kuwa na maeneo bora zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *