Muigizaji wa Bongo Movie, Wema Sepetu na wenzake wawili wanatarajiwa kusomewa mashtaka yao ifikapo Julai 10 mwaka huu.
Wema na wenzake wanakabiliwa na kesi ya kukutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.
Wema na wenzake, Angelina Msigwa na Matrida Abas walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa mawili likiwamo la kukutwa na kiasi kidogo cha dawa za kulevya.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde, alidai mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.
Wema Sepetu ni miongoni mwa wasanii waliotajwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wanaojihusisha na masuala ya dawa za kulevya.