Muigizaji wa Bongo Movie, Wema Sepetu amefunguka na kusema kuwa huwa anajisikia vibaya akiwaona watoto wa mastaa wenzake.
Wema anasema kuwa, hakuna kitu kinachomuumiza kila kukicha kama kuona marafiki zake kama Irene Uwoya, Aunt Ezekiel, Lulu na Jacqueline Wolper wakiwa na watoto wao, lakini yeye bado hajabahatika.
Wema anasema kuwa, kuna muda anajisahaulisha kuhusiana na kupata mtoto, lakini baada ya muda kinatokea kitu kinachomkumbusha.
“Naanza kuumia sana na ndiyo hali inayonikuta nikiwa na marafiki hao,” anasema Wema ambaye ni mmoja wa memba wa kundi la mastaa hao wanaojiita Big Six na kuongeza;
“Yaani mimi naumia sana, natamani sana kusahau hili, lakini ukweli ni kwamba kuna muda natamani na ninapoona rafiki zangu wanawaongelea watoto wao; yaani kama mwanadamu naumia na mimi natamani kubeba mtoto wangu.”
Kwa miaka mingi Wema amekuwa akitoa kilio chake cha kukosa mtoto na amekwishakwenda kwenye matibabu bila mafanikio.