Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy amevitaka vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali za serikali kuacha tabia ya kuuza dawa za kutibu malaria nchini.
Waziri Ummy amesema hayo wakati alipotembelea Zahanati ya Mwandiga iliyopo wilayani Kigoma Mkoa wa Kigoma katika akiwa anangalia hali ya matibabu dhidi ya malaria wilayani humo kuelekea kilele cha siku ya Malaria Duniani.
Waziri Ummy amewataka waganga wakuu wa vituo ngazi za zahanati na waganga wakuu wa wilaya waweke namba zao za simu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kuwasaidia Watanzania kutoa malalamiko yao pindi wanapopatiwa huduma ambazo za hazikidhi viwango ili kubendelea kuboresha huduma za afya nchini.
Waziri Ummy amesema kuwa katika kujikinga na Malaria wananchi wanatakiwa kutumia vyandarua vyenye dawa, kusafisha mazingira na kuondoa mazalia ya mbu waenezao ugonjwa huo kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Pia Waziri Ummy ametoa vyandarua vyenye dawa ya kukinga dhidi ya Malaria katika kijiji cha Mwandiga ili kuendelea na juhudi za kutokomeza Malaria nchini katika kuelekea siku ya Malaria Duniani.