Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameendelea kusisitiza kuwa wananchi hawapaswi kununua damu kwani huduma hiyo ni bure kwa watanzania wote katika hospitali zote.

Waziri Ummy amesema leo wakati wa uzinduzi wa Benki ya damu iliyodhaminiwa na Ubalozi wa Kuwait katika Taasisi ya Mifupa MOI ambapo uliuzuliwa na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa wananchi wanatakiwa kujitokeza katika kuchangia damu ili kuweza kuwa na hifadhi ya kutosha na kufanya kazi kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kwa wakati sahihi bila ya usumbufu wowote katika kuokoa maisha ya watanzania.

Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa anayo furaha kutimiza miaka miwili tangu kuingia kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kupiga hatua katika sekta ya afya hasa katika kupunguza rufaa za nje na kuwa na utaalamu wa matibabu ya kibingwa kama vile upandikizaji wa figo, vifaa vya usikivu( Coclea Impant) na kutibu magonjwa ya moyo.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania Bw. Jasem Ibrahim Al-Najem amesema kuwa wameamua kuchangia kiasi cha fedha cha shilingi Milioni 200 katika kutengeneza Benki hiyo ya damu MOI ili kuweza kusaidia kuboresha sekta ya afya nchini.

Aidha katika uzinduzi huo wa Benki ya damu Balozi Al-Najem alijitolea damu unit moja ili kuweza kuchangia benki hiyo ya taasisi ya Mifupa MOI ili kuweza kuhamasisjha na wananchi wengine waweze kuchangia damu kwa msaada wa wagonjwa wengine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Lwezimula alisema kuwa katika kuhakikisha Matibabu ya kibingwa yanapiga hatua nchini waliamu kuanzisha kambi za matibabu kuanzia mwaka 2000 na kufanya taasisi zingine za afya kuiga mfano huo.

Sambamba na tukio hilo Kikundi cha Kutayarisha Madereva wa Magari Makubwa Wanawake (WOW) Afrika Mashariki walijitolea kuchangia damu ili kuweza kusapoti benki hiyo kwa ajili ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo ya damu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *