Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba amesema watanzania wengi hawali nyama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa virutubisho vya protini vilivyomo kwenye nyama.
Dkt. Tizeba amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa wingi wa ng’ombe barani Afrika lakini ulaji wa nyama kwa wananchi wake ni mdogo sana jambo linalosababisha wananchi wengi kuwa na mifugo mingi ambayo kwa upande wa afya wengi hawaifaidi.
Aidha waziri huyo amewataka wafugaji kuondokana na dhana ya kufuga mifugo mingi katika eneo dogo huku wakiwa hawana uhakika na soko la mifugo hiyo jambo linalofanya mifugo mingi kusafirishwa umbali mrefu na mwisho wa siku inakuwa inakosa ubora unaotakiwa.
Pia waziri ametumia fursa hiyo kukemea uvuvi haramu ambapo amesema samaki mmoja anaweza kuvuliwa akiwa na mayai milioni 6 tumboni na kushangiliwa na wateja lakini mvuvi huyo anaweza kuwa ametumia nyavu zinazokatazwa au sumu jambo ambalo tukiliacha kwa muda mrefu litafanya maziwa yetu yakose samaki kabisa.
Vile vile waziri huyo amesema kuna watafiti wamemueleza kuwa sumu inayotumika kuulia samaki siyo kwamba ina athari kwa samaki tuu bali kwa wanadamu ni kubwa na kwa upande wa wanaume inaharibu unyumba kabisa.