Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewaonya waumini wa dini mbalimbali nchini kutotumia mwamvuli wa dini kufanya vitendo vya uhalifu.
Nchemba ametoa kauli hiyo jana alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka lililofanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mwigulu amesema serikali inatambua uhuru wa kuabudu iliyoutoa kwa wananchi wake na inaunga mkono kazi nzuri inayofanyika kupitia ibada, lakini uhuru huo usikwaze wengine, na wala usivunje sheria.
Katika hatua nyingine, Waziri Nchemba ameagiza taasisi zilizo chini ya wizara yake kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada, badala ya kuwapa njia ngumu kwani nyumba hizo ni muhimu kwa ajili ya kumuombea Rais Magufuli na taifa kwa ujumla
Pia amewataka waumini wa dini mbalimbali kuendelea kuliombea taifa, huku akiwapongeza kwa kazi nzuri ya maombi waliyoifanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Waziri Mwigulu pia alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wasanii wa nyimbo za injili kuwa serikali itafanya kila iwezalo kulinda maslahi ya kazi zao.