Ofisi za lebo ya muziki nchini Wasafi Classic Baby maarufu kama WCB zimetembelewa na waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kufanya mazungumzo na wanamuziki wa lebo hiyo akiwemo Diamond Platnum.
Uongozi wa lebo hiyo umemuomba waziri huyo kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kupunjwa mapato yatokanayo na miito ya simu (Caller tunes) pamoja na wizi wa kazi za wasanii.
Pia uongozi wa lebo hiyo umemuomba Waziri Nape kuwawezesha kupata eneo (Ukumbi wa Kisasa) kwa ajili ya kufanyia maonesho makubwa ya musiki, wasanii kupata elimu juu ya kulipa kodi kwa kazi zao na kuongeza kiwango cha uwiyano kwa nyimbo za kitanzania zinazopigwa redioni dhidi ya nyimbo za kigeni.
Kwa upande wake Waziri , Nape Moses Nnauye amehaidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na kuifanya tasnia ya muziki kuwa ajira kubwa kwa vijana wengi kwa kuongeza vipato vyao na pato la taifa kwa ujumla.
Hiyo ni mara ya pili kwa kiongozi wa Serikali kuitembelea lebo hiyo baada ya siku za nyuma kutembelewa na Waziri anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira, January Makamba.
Lebo hiyo ya muziki wa Bongo fleva nchini inamilikiwa na Mwanamuziki maarufu wa Bongo fleva Diamond Platnum akiwa chini ya mameneja, Babu Tale na Salam SK.
Picha kwa hisani ya Global Publishers