Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema kuwa kitendo cha kumkabidhi bendera Diamond kwa ajili ya kwenda kutumbuiza kwenye ufunguzi wa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Gabon ni jambo ambalo lipo sahihi.
Kauli hiyo ya waziri Nape imekuja baada ya watu kusema kuwa kitendo hicho cha wizara ya habari kumkabidhi bendera Diamond siyo sahihi kutokana na mwanamuziki huyo aendi kuiwakilisha nchi bali anakwenda kwa maslai yake binafsi.
Waziri Nape amesema kuwa ameshangazwa na kelele hizo huku akisema kuwa watanzania huwa wanapenda kuhangaika na vitu vya kijinga visivyokuwa na maana kwani kufanya hivyo si kosa kutokana kila anayekwenda kufanya jambo kubwa nje ya nchi ana haki ya kukabidhiwa bendera ya taifa.
Nape amemtolea mfano mwanamuziki Shakira aliyetumbuiza kombe la dunia nchini Afrika kusini mwaka 2010 alikuwa na bendera ya nchi yao.
Siku ya jumanne Waziri Nape alimkabidhi bendera ya taifa Diamond Platnumz kwa ajili ya kwenda kutumbiza kwenye ufunguzi wa michuano ya mataifa ya Afrika yatakayofanyika nchini Gabon kuanzia kesho.