Serikali imesema itahakikisha inachukua hatua zote ili kuhakikisha kiwango cha bajeti ya maendeleo kilichotengwa kinatolewa kwa wakati na kinatekelezeka.
Katika mwaka wa fedha 2017-18 Serikali imetenga bajeti ya Sh32 trilioni na kati ya hizo Sh11.9 kitakwenda katika sekta ya maendeleo.
Akisoma mwelekeo wa hali ya uchumi wa taifa bungeni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema kwa vile Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kukuza sekta ya viwanda, itasimamia jambo hilo litekelezwe kwa kuhakikisha kiwango cha fedha kwa ajili ya maendeleo kinatolewa kwa wakati.
Kwa miaka kadhaa kumekuwa na malalamiko juu ya kutotolewa kwa kiwango chote cha bajeti ya maendeleo licha ya mpango huo kupitishwa na Bunge.
Lakini Waziri Mpango ameahidi kutolewa kwa fedha hizo kwa wakati na kudai kuwa katika kutekeleza hilo Serikali inakusudia kuanzisha vyanzo vipya vya mapato.
Pamoja na kuanzisha vyanzo vipya ya ukusanyaji mapato, Serikali inakusudia kufanyia mabadiliko mfumo mzima wa ukusanyaji kodi ambao utahakikisha mapato hayo yanakusanywa kwa ufanisi kwa wigo mpana.