Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kwamba wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi wanaiathiri Serikali katika juhudi zake za kuboresha maisha ya Watanzania.
Amesema Serikali haina mgogoro na wafanyabiashara bali inawataka walipe kodi na kama kuna wanaoonewa na watendaji wa chini kwa kubambikiziwa kodi watoe taarifa juu ya jambo hilo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohamed Dewji, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imedhamiria kuwaunga mkono wafanyabiashara katika shughuli zao ili waweze kulipa kodi itakayoifanya imudu kuwahudumia wananchi katika huduma mbalimbali za jamii.
Pia amewataka wafanyabiashara kwenda kujenga viwanda katika maeneo ambayo malighafi zinazalishwa ili kuwahamasisha wakulima kuzalisha zaidi na kuwapunguzia mzigo wa kusafirisha malighali hizo.
Kwa upande wake Dewji amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wafanyabiashara wanaiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano na hawana mpango wowote wa kuhamishia mitaji yao nje ya nchi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Amesema yuko tayari kuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda cha sukari katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kununua miwa tani milioni 1.2 zitakazozalisha tani 120,000 za sukari kwa mwaka.
Mohameda Dewji amesema amepanga kuwekeza sh. bilioni 40 kwa ajili ya kukuza uzalishaji katika mashamba yake ya mkonge kwenye mikoa ya Pwani, Tanga na Morogoro.
Pia amewekeza sh. bilioni 70 katika viwanda vya kusaga unga wa ngano na sembe na anatarajia kununua tani laki moja za mahindi katika msimu wa mwaka huu.
Mbali na kuwekeza katika viwanda hivyo Dewji amesema anatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza sabuni ya unga ambacho kitakuwa ni kikubwa kuliko vyote katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.