Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amesema ana imani na Rais Mteule wa Marekani Donald Trump na kwamba wawili hao wanaweza kuaminiana.
Abe ameeleza mkutano wa dakika 90 kati yake na Bw Trump katika jumba la Trump Tower, New York, kama wa uwazi na wa kirafiki.
Wakati wa kampeni, Bw Trump alitilia shaka manufaa ya urafiki kati ya Marekani na baadhi ya washirika wake wa muda mrefu, ikiwemo Japan.
Mkutano huo ulikuwa wa kwanza wa ana kwa ana kati ya Trump na kiongozi wa nchi nyingine duniani tangu ashinde urais.
Marekani na Japan zimekuwa washirika wakubwa tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ambapo Marekani iliisaidia Japan kufufua tena uchumi wake.
Trump ameahidi kufuta mktaba wa kibiashara kati ya Marekani na nchi za Pasifiki, ambapo Bw Abe amekuwa wakiuunga mkono sana kama njia ya kukabili ubabe wa kiuchumi wa China.