Waziri Mkuu wa Jamhri ya muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mabadiliko ya mifumo ya ujenzi wa uchumi wa viwanda hayawezi kuletwa na Serikali peke yake bali ni lazima yahusishe pia wadau kutoka sekta binafsi.

Ametoa kauli hiyo wakati akichangia mjadala kuhusu TICAD na umuhimu wake kwa maendeleo ya Afrika mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI) uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi nchini Kenya.

Waziri Mkuu amehudhuria mkutano huo wa siku mbili kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, amesema Tanzania inawakaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kutoka Japan waje kujenga viwanda vya kusindika gesi asilia, kutengeneza mbolea na kemikali mbalimbali, vyuma, nguo, bidhaa za ngozi na usindikaji wa mazao.

Pia amesema ili kufikia uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu, ni lazima nchi za Afrika na wabia wa TICAD wawekeze kwa pamoja na washirikiane kujenga uwezo wa rasilimali watu, kwa kuwa ndio nguzo muhimu ya kuleta ushindani wenye tija katika sekta ya viwanda.

Waziri Mkuu wa Japan, Bw. Shinzo Abe aliwaahidi viongozi wa nchi za Afrika kwamba nchi yake itatoa kiasi cha dola za marekani bilioni 10 katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuendeleza miundombinu barani humo na kwamba sehemu ya fedha hizo itatolewa kwa kushirikiana na Benki ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).

Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano wa TICAD kufanyika barani Afrika tangu mikutano hii ianze mwaka 1993.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *