Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa inatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia mwezi ujao baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji.
Mradi huo unajengwa kwa usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga (SUWASA), kwa ufadhili wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya Maendeleo (KfW) sh. bilioni 31 utakapokamilika.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati na akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Sumbawanga na kuitaka kampuni ya kampuni ya Techno Fab Gammon Joint Venture ya India kumaliza ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.
Waziri mkuu amesema mradi huo ambao tayari umekamilika kwa asilimia 85 unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Manispaa katika kulinda miundombinu ya mradi huo mara utakapokamilika pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
Pia alisema kumekuwa na uvamizi mkubwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo wananchi wanajishughulisha na shughuli za ulimaji, uchungaji wa mifugo, ujenzi wa nyumba za makazi na uchomaji misitu hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira na hatimaye vyanzo hivyo hukauka.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wote wa wilaya na wenyeviti wa vijiji nchini kuyasimamia maeneo yenye vyanzo vya maji na kuwaondoa watu wotewalioyavamia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwafikisha mahakamani.
Kwa upande mwingine Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye alimuwakilisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge katika hafla hiyo amesema aliishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa nchi za Ulaya kwa kufadhili mradi huo.