Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa anahamia mjini Dodoma leo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ahadi ya Serikali ya awamu ya tano ya kuhamia Dodoma.

Julai 25 mwaka huu, katika kilele cha siku ya mashujaa kilichofanyika Dodoma Waziri Mkuu Majaliwa alisema ifikapo Septemba mwaka huu, Serikali itakuwa imehamia mjini Dodoma.

Hatua hiyo ya  waziri mkuu  ilitangazwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alipozungumza  na waandishi wa habari.

Alisema, “ Waziri Mkuu anatarajiwa kuwasili leo mchana akitokea   Dar es Salaam alikokuwa akiishi. Baada ya kuwasili hapa  atafanya ziara ya siku mbili katika Manispaa ya Dodoma Oktoba mosi na Oktoba 2 mwaka huu   kukagua hatua mbalimbali za maandalizi ya kupokea   Serikali mkoani hapa.

“Wakati wa ziara hiyo, atakagua majengo ya Serikali, maeneo ya kutolea huduma za afya, kituo cha umeme cha Zuzu, masoko, chanzo cha maji Mzakwe na maeneo ya viwanda.

“Kwa hiyo  maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mapokezi ya waziri mkuu yamekamilika na uongozi wa mkoa unaendelea kuwajulisha wananchi na wadau wote katika maeneo yatakayohusika na ziara hiyo, washiriki kwa ukamilifu.

“Kwa niaba ya uongozi wa Mkoa wa Dodoma, tunampongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuitikia na kutekeleza uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa kuhamia makao makuu mjini hapa.”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *