Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Ruvuma.

Waziri Mkuu atawasili leo mjini Songea na kupokelewa na viongozi wa Chama na Serikali katika Uwanja wa ndege Songea majira ya 7.00 mchana.

Baada ya kuwasili atapokea taarifa ya maendeleo ya Mkoa na ile ya Chama Tawala Uwanja wa Ndege Songea. Kisha ataelekea Wilaya ya Namtumbo ambapo atafungua ghala la MIVARF, kuongea na Madiwani na watumishi wa Umma na baadaye ataongea na wananchi wa Namtumbo kwenye mkutano wa hadhara.

Kesho Waziri Mkuu ataendelea na ziara yake kwa kuongea na wananchi wa kijiji cha Mchomoro kisha ataelekea Wilaya ya Tunduru ambapo atasalimia na wananchi wa vijiji vya Rahaleo,Milonde na Matemanga akiwa njiani kuelekea mjini Tunduru.

Waziri Mkuu atatembelea kituo cha Afya cha Nakayaya, ghala la kuhifadhia Korosho na kupata taarifa ya Chama Kikuu Cha Ushirika TAMCU. Jioni Waziri Mkuu ataongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika mjini Tunduru katika uwanja wa michezo. Jumamosi tarehe 25 Novemba, 2017 Mheshimiwa Waziri Mkuu atahitimisha ziara yake mkoani Ruvuma na kurejea Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa Mndeme ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi katika mapokezi kuanzia uwanja wa Ndege Songea atakapowasili.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *