Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji katika kijiji cha Bwasa katika mji wa Nansio wilayani Ukerewe.

Waziri Mkuu alizindua mradi huo jana (Jumapili, Februari 18, 2018) wakati akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Alisema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini.

Baada ya kuzindua mradi huo, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi wa mji wa Nansio kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Getrude Mongella, ambapo alisema mradi aliouzindua katika kijiji cha Bwasa ni sehemu ya mradi wa maji wa Kazilankanda utakaohudumia vijiji 13 vya wilaya hiyo.

Alisema mradi huo unagharimu shilingi bilioni saba na unatekelezwa katika vijiji vya Muhula, Mahande, Namasabo, Namagondo, Kazilankanda, Malegea, Igalla, Kigara, Lutare, Busunda, Bwasa, Buhima, Hamuyebe  na utahudumia wakazi  68,038 pindi utakapokamilika.

Mkataba wa Mradi huo ulisainiwa Machi 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo April, 2018, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 5.637 sawa na asilimia 78.26 tayari zimeshatumika na mradi umekamilika kwa asilimia 92 na tayari baadhi vijiji vimeanza kupata maji.

Waziri Mkuu alisema mkakati wa Serikali ni kuwahudumia wananchi kwa kutatua kero zinazowakabili ikiwemo ya upatikanaji wa maji, ambapo imedhamiria kuendelea kusambaza huduma hiyo hadi vijijini ili kuhakikisha vyote vinapata maji.

Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *