Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania Russia na Rwanda kutumia fursa hiyo kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali, ikiwamo ya utalii.

Pia amewataka Mabalozi kila mwisho wa mwaka wajifanyie tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika mataifa wanaiwakilisha nchi ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayewakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayewakilisha Tazania nchini Russia, katika ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

Waziri Mkuu alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii pamoja na uwapo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia katika kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii nchini.

Alisema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

Pia Waziri Mkuu aliwataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanazoiwakilisha ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi na wakumbuke nyumbani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *