Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewapa mwezi mmoja watumishi wa umma ambao hawajaripoti kwenye kituo chao cha kazi katika Wilaya mpya ya Kibiti, mkoani Pwani kufika mara moja na kuanza kazi.

Agizo hilo alilitoa jana wilayani Kibiti akiwa kwenye ziara yake mkoani Pwani kukagua shughuli za maendeleo, utekelezaji wake na kueleza msimamo wa serikali kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Alvera Ndabagoye alimwambia Waziri Mkuu kuwa hadi sasa wilaya hiyo ina watumishi nane walioripoti kati ya watumishi 74.

Aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mkuu wa Idara ya Uhasibu, wahasibu wawili, madereva wawili, Katibu Muhtasi na Ofisa Utumishi.

Waziri mkuu amesema watumishi wote waliopangwa kufanya kazi katika wilaya hiyo,wanapaswa kuwepo ndani ya eneo hilo na kuwatumikia wananchi na kama kuna changamoto zinapaswa kushughulikiwa wakiwa kazini.

Akifafanua zaidi, alisema changamoto za ukosefu wa nyumba za kuishi ni mambo yanayoweza kutafutiwa ufumbuzi wakati watumishi hao wakiwa kwenye eneo la kazi na kuwataka uongozi wa wilaya hiyo kuzungumza na Mifuko ya Hifadhi za Jamii na kuingia nao mikataba kuona jinsi watakavyojenga nyumba za makazi.

Akizungumzia majengo ya ofisi ya wilaya hiyo, Mkurugenzi Ndabagoye alisema kuna uhaba wa majengo ya ofisi wilayani Kibiti kutokana na upya wa wilaya hiyo lakini pamoja na hali hiyo yeye na watumishi hao wachache wamesharipoti kazini na kuanza kazi.

Awali akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo,Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao kutumia nafasi zao kwa manufaa ya nchi kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuibadilisha wilaya hiyo.

Akisoma taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gulamhussein Kifu alisema pamoja na mafanikio yaliyopo bado kuna changamoto zikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji,uvuvi haramu, miundombinu na uhaba wa watumishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *