Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaomba Viongozi wa Jumuiya na Taasisi zote za kidini nchini wahakikishe wanawapiga vita watu wote wanaopanga na kutaka kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini kwa sababu watakwamisha maenendeleo.
Amesema Serikali inaelewa kwamba dini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya maendeleo ya ustaarabu wa mwanadamu kwani inatoa elimu ya maadili mema yenye kuwafanya waumini waepukane na maovu mbalimbali.
Majaliwa ametoa kauli hiyo Oktoka 01, 2017 wakati akifungua mkutano Mkuu wa mwaka wa 48 wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya uliofanyika katika eneo la Kitonga kata ya Msongola wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Amesema iwapo dini zetu zitatumika vizuri tutaweza kwa haraka sana kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Magufuli la ‘Hapa kazi tu’ kwani kila mtu ataepuka uzembe na kuwajibika ipasavyo.
Majaliwa amesema ana imani kwamba jumuiya hiyo kama zilivyo taasisi zingine za kidini itaendeleza kazi kubwa ya kupambana na maovu katika jamii yetu kwa kuwapatia waumini wao na wananchi kwa ujumla elimu na maarifa ya kuboresha tabia zao na maadili yao kiroho.
Amesema amani na utulivu uliopo nchini unatokana na mambo mengi ikiwemo na wananchi kupata ustawi, kuweza kufanya shughuli zao vizuri na kuwa na imani na Serikali yao, ambayo imejiwekea mikakati ya kuhakikisha wananchi hususan wanyonge wanapata faraja ndani ya nchi yao.
Amesema mambo yameweza kupatikana baada ya Serikali kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuimarisha maadili ya watumishi wa umma, ambayo vimekuwa ni vyanzo vya kupotea kwa amani na utulivu katika baadhi ya nchi.