Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameuvunja Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Kahawa (CDTF).
Pia waziri mkuu amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza mwenendo wa mfuko huo tangu ulipoanzishwa.
Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wadau wa zao hilo kwenye kikao cha kujadili maendeleo ya zao la kahawa alichokiitisha, mjini Dodoma.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kwamba uundwaji wa mfuko huo si wa kisheria bali ni wadau wa zao hilo kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).
Pia aliagiza kufungwa kwa ofisi za CDTF ili kupisha uchunguzi na baada ya CAG kukamilisha uchunguzi na kukabidhi ripoti, kazi zote zilizokuwa zinafanywa na mfuko huo zitafanywa na Bodi ya Kahawa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa majukumu ya kuundwa kwa mfuko huo yanaingiliana na yale ya Bodi ya Kahawa, ambayo ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya zao hilo, hivyo hakuna haja ya kuwa vyombo viwili vinavyofanya kazi moja.