Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekemea vitendo vya uvuvi haramu wa kutumia sumu kali ndani ya ziwa Victoria kwa sababu vinaharibu soko la samaki.
Aliyasema hayo jana jioni (Jumamosi, Februari 17, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisorya wilayani Bunda mkoani Mara.
Alisema kitendo cha kuvua kwa kutumia sumu kinaharibu soko la samaki la ndani na nje ya nchi kwa sababu sumu hiyo inabaki hivyo kumuathiri mlaji.
Waziri Mkuu aliwaagiza Maofisa Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenda kutoa elimu kwa wavuvi wa eneo hilo juu ya madhara ya zana haramu za uvuvi.
Alisema baadhi ya wavuvi wanavua kwa kutumia nyavu zilizopigwa marufuku, kokoro pamoja na mabomu jambo ambalo haliwezi kuvumilika kwa sababu zana hizo zinaharibu uhai wa viumbe hai ndani ya ziwa Victoria.
Pia, Waziri Mkuu alisema Serikali tayari imeshaagiza nyavu zinazofaa kwa ajili ya uvuvi endelevu kutoka nje ya nchi ambazo zitauzwa kwa wavuvi mbalimbali.
Waziri Mkuu alisema wavuvi wote wanatakiwa kufuata sheria ikiwemo kuwa na leseni za uvuvi kwa vyombo vyao, hivyo alimuagiza Afisa Uvuvi afanye ukaguzi.
Alisema Serikali inafanya uhakiki wa vyombo na wavuvi wote ili kubaini nani anavua wapi na kwa utaratibu upi. “Kamati ya Ulinzi na Usalama simamieni suala hili.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Amos Kusaja kuhakikisha gari la kuhudumia wagonjwa la Kituo cha Afya cha Kasahunga linakuwa na mafuta wakati wote.
Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliodai kuchangishwa fedha za mafuta ya gari hilo mara wagonjwa wao wanapopewa rufaa kwenda katika hospitali ya wilaya.