Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.
Waziri Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo kwa Taifa ni jambo muhimu.
Kutokana na hali hiyo Serikali inawasisitiza Wananchi kuwa wazalendo na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini zinaendelezwa.
Amesema Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili kufanikisha adhma hiyo.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao kuzingatia sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani mara wamalizapo masomo yao.
Amesema Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo yao.