Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano, Kassim Majaliwa amepokea zaidi ya Sh milioni 379 na vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 280 kutoka kwa taasisi saba tofauti kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa maafa ya tetemeko mkoani Kagera.
Vifaa vilivyotolewa ni mahema 220, blangeti 1,100, magodoro 1,100, chupa za maji 250, mikeka 22, nguo na unga tani 10.
Majaliwa akipokea msaada huo, alizishukuru taasisi hizo kwa msaada huo walioutoa kwa lengo la kuwachangia Watanzania waliopatwa na maafa hayo.
Amesema mpaka sasa wanaendelea kusubiri muda wa kutamka kiwango walichopata na kazi zinazoendelea katika eneo hilo la Kagera.
Amesema serikali inaendelea kuratibu michango yote, inaendelea kusimamia vizuri michango hiyo, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi. Aidha, Waziri Mkuu alivishukuru vyombo vya habari ambavyo vimeendelea kuhamasisha Watanzania wengine kuchangia.
Amesema kwa wale watakaokuwa tayari kutoa misaada yao jijini Dar es Salaam ataipokea Oktoba 14 saa sita mchana.
Taasisi zilizotoa msaada huo ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Sh milioni 41.5, Sura Technology Sh milioni tano, Magereji Tegeta Sh milioni mbili, Wakaguzi wa Ndani Sh milioni 6.7, wafanyabiashara Kariakoo Sh milioni 60, Ubalozi wa Japan Sh milioni 220 na Acacia Sh milioni 325.