Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, kupiga kambi katika Kata ya Miono wilayani Bagamoyo ili kuwasaka wafugaji wanaodaiwa kuwapiga wakulima.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana, Majaliwa alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kata hiyo ambao walisimamisha msafara wake wakati akienda kukagua miundombinu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyoko wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Akitoa kero za eneo hilo, Diwani wa Kata ya Miono, Juma Mpwimbwi, alisema kata hiyo inakabiliwa na tatizo la wakulima kupigwa na wafugaji na wakipelekwa kituo cha polisi hawachukuliwi hatua yoyote.

 Pia alisema mbali ya kero sugu ya maji, waliahidiwa barabara ya lami tangu miaka saba iliyopita lakini hadi sasa hawana hata kipande kidogo tu cha barabara hiyo.

Aliwataka wafugaji wanaokata mabomba ya maji ya mradi wa maji wa Chalinze (Chaliwasa) ili kupata maji ya kunywesha mifugo yao, waache tabia hiyo mara moja na akaonya kuwa watakaokamatwa, wachukuliwe hatua za kisheria mara moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *