Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Bw. Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa wengine watatu.

Waziri Mkuu amewasimamisha kaimu mkurugenzi huyo wakati alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.

Pia Waziri mkuu amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Songwe, Bw. Damian Sutta kuwakamata na kuanza kuwachunguza haraka Maofisa hao na kisha ampelekee taarifa ofisini kwake.

Waziri Mkuu aklisema “hatuwezi kuendesha Serikali kwa namna ambayo haikubaliki kwani watu tuliowapa dhamana ndio wanaongoza kwa vitendo vya rushwa na ufisadi. Wameifanya Halmashauri hii kama shamba la bibi.”

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mheshimiwa Eric Ambakisye kuhakikisha anasimamia vizuri utendaji ndani ya Halmashauri hiyo na kwamba Serikali inataka watu waadilifu na wenye uaminifu na nidhamu.

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa dhamana wakijinufaisha kwa fedha za umma na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za maji, afya na elimu, hivyo itaendelea kuwachukulia hatua.

Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Bw. Simon Noel, Bw. Bahati Chomoka ambaye ni Cashier na Bw. Remmy Haule ambaye ni Ofisa Ugavi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *