Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini.
Amesema mkakati wa Serikali ni kuimarisha uchumi hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo alipokutana na mabalozi wa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italy, Ufaransa, Jamuhuri ya Kidemkrasi ya Congo (DRC) na Uswisi.
Mabalozi hao ni Balozi Dk. Emmanuel Nchini (Brazil), Balozi Elizabeth Kiondo (Uturuki), Balozi George Madafa (Italy), Balozi James Msekela (Uswisi),Balozi Samuel Shelukindo (Ufaransa), Balozi Paul Mella (DRC), Balozi Mbelwa Kairuki (China).
Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao kuhakikisha wanawatambua Watanzania wanaoishi katika mataifa hayo na kushirikiana nao katika kutafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Balozi Mella ambaye alizungumza kwa niaba ya mabozi wenzake alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watakwenda kutekeleza wajibu wao ipasavyo