Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amekagua mradi wa usambazaji wa maji kwenye vijiji vinavyopitiwa na mradi wa maji Mbwinji na ameridhishwa na unavyoendelea.
Waziri Mkuu alifanya ukaguzi huo katika kioksi cha kuchotea maji kilichopo kwenye kijiji cha Mbecha wilayani Ruangwa na kusema mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea (MANAWASA) unatarajiwa kukamilika Machi 31, 2018.
Aidha, Waziri Mkuu amesema vijiji ambavyo vimenufaika na mradi huo wilayani Ruangwa ni sita ambavyo ni Chiyapi, Nandanga, Ipingo, Lucheregwa, Litama na Mbecha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MANAWASA Mhandisi David Mwamsojo amesema mradi huo utagharimu sh. milioni 870.738 hadi kukamilika na kuhusisha vijiji 12 vilivyo kwenye umbali wa kilomita tano kutoka kwenye bomba kuu pamoja na ujenzi wa vioksi 18 vya kuchotea maji.