Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameugiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumpelekea nyaraka zote zilizotumika katika kumhamisha faru maarufu kwa jina la John katika hifadhi hiyo ifikapo kesho.
Majaliwa amesema ana taarifa kuwa walimhamisha Faru John Kreta kwa siri na kumpeleka V I P Grumet Serengeti Disemba 17, 2015 na waliahidiwa kupewa sh. milioni 200 ambapo na wamepewa sh. milioni 100 kwa ahadi ya kumaliziwa sh. milioni 100 nyingine baadaye.
Amesema hayo Desemba 6, 2016 alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA, zilizoko wilayani Ngorongoro mkoa Arusha wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Aidha, Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ambao wanawakabidhi watoto kupeleka ng’ombe wao ndani ya kreta.
Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanafanyakazi kwa kufuata misingi ya kiutumishi na kuacha tabia za kuendekeza rushwa na wizi.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa NCAA, Sezzary Simfukwe kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na tayari anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).