Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Uledi Mussa afuatilie malipo ya kiwanja kilichouzwa na CDA kwa Sh milioni 240 huku fedha iliyoingia ofisini ni milioni sita tu.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) kwenye ukumbi wa Hazina Ndogo, mjini Dodoma.
Majaliwa amesema eneo hilo lilipaswa kuwa na kituo cha mafuta na akataka apatiwe taarifa mapema iwezekanavyo.
Pia alimwagiza Katibu Mkuu huyo, afuatilie mkataba wa upangishaji wa jengo la CDA ambalo Taasisi ya Tunakopesha Limited, imepangishwa kwa madai kuwa mhusika alipewa bure , lakini sasa anataka kulipangisha tena ili apate cha juu.
Amesema jumla ya viwanja 70,000 vimepimwa tangu CDA ianzishwe mwaka 1973 na kama wataendelea na kasi hiyo wakati mahitaji yameongezeka, itawachukua zaidi ya miaka 40 kukamilisha mahitaji ya viwanja 100,000, ambavyo vinatarajiwa kuanza kupimwa hivi karibuni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili, amesema usanifu wa upimaji viwanja 20,000 umekamilika na kwamba wana lengo la kupima viwanja vingine 100,000 ifikapo Juni 2017.