Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Sumitomo Mitsui anayejenga barabara ya juu eneo la Tazara jijini Dar es Salaam kuongeza kasi ya ujenzi huo ili kupunguza muda wa ujenzi wa mradi huo.
Nguzo 46 kati ya 63 zinazohitajika kwenye awamu ya kwanza ya ujenzi, zimeshasimikwa ardhini.
Akizungumza katika eneo la ujenzi huo, Profesa Mbarawa amepongeza hatua iliyofikiwa, lakini amesisitiza kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili wananchi wanufaike.
Mradi huo uliozinduliwa Desemba Mosi, 2015 umekamilika kwa asilimia 25.3 na zaidi ya Sh bilioni 96.5 zinatarajiwa kutumika hadi utakapokamilika Oktoba, 2018.
Pia waziri huyo amewataka wafanyakazi katika mradi huo kuongeza bidii na uaminifu kazi kwa kuwa serikali ina mpango mwingine wa kujenga barabara kama hiyo itakayowawezesha kupata tena fursa ya ajira.
Naye Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida amemhakikishia waziri Mbawara kuwa ujenzi wa mradi huo utamalizika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo kusaidia kuondoa msongamano katika barabara za Nyerere na Mandela.