Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amempa miezi kumi Mkandarasi wa Kampuni ya CICO anayejenga barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30 kwa kiwango cha lami kukamilisha kazi hiyo.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo mkoani Tabora mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kuelezea kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake.
Mbarawa amesema “Nakupa miezi kumi tangu sasa hadi mwezi Mei mwakani uwe umeikabidhi Serikali barabara hii”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa ukamilishaji wa barabara hiyo uendane na viwango na ubora vinavyoendana na thamani ya fedha waliyopewa ili barabara hiyo iweze kudumu kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mwalimu Queen Mlozi, amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa kuufuatilia kwa karibu mradi huo ambao utachochea kasi ya maendeleo mkoani humo.