Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi anayejenga Reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge) sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro kilomita 205 kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya miezi thelathini iliyopangwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua tuta litakapojengwa reli hiyo kutoka pugu, soga hadi ngerengere profesa mbarawa amepongeza kazi inayoendelea na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kazi ya kutandika reli ianze katika muda mfupi ujao.
Profesa Mbarawa amekagua kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege yatakayotumika katika ujenzi wa reli hiyo na kusisitiza umuhimu wa mkandarasi kutoa fursa za ajira kwa wananchi wanaozunguka reli hiyo.
Profesa Mbarawa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli (TRL) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli RAHCO) Bwana Masanja Kadogosa kuanza mchakato wa kuagiza vichwa vipya vya treni vinavyowiana na Reli hiyo ili reli itakapokamilika kusiwe na hoja ya kusubiri vichwa hivyo.
Aidha amesisitiza umuhimu wa TRL na RAHCO kuandaa wataalam watakaotumika kuendesha Reli hiyo ya kisasa kwa kuwapatia mafunzo ya kiufundi na kibiashara ili kuhakikisha utendaji wa Reli hiyo unakuwa wenye tija.
Ujenzi wa Reli ya kisasa ya kati (Standard Gauge) awamu ya kwanza inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa Kilomita 205 unatarajiwa kukamilika 2019 na Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha inapata fedha ya Ujenzi wa sehemu ya Morogoro-Dodoma.
Zaidi ya Kilomita 2600 za Reli ya Kisasa (Standard Gauge) ZINATARAJIWA kujengwa kutoka Dar es Salaam –Morogoro-Dodoma –Tabora-Isaka-Mwanza na Tabora –Kaliua-Kigoma ili kuiunganisha Tanzania nan chi jirani na hivyo kuboresha huduma za uchukuzi na biashara.