Waziri wa nchi ofisi ya rais, utumishi na utawala bora, Angela Kairuki amesema serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na madaktari, matabibu pamoja na wauguzi nchini.
Ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma, akijibu swali la mbunge wa viti maalum Zubeda Hassan Sakuru, lililosema: kumekuwepo na vifo visivyokuwa vya lazima kutokana na kutokuwepo kwa motisha kwa madaktari na wauguzi kwa kulipwa viwango duni vya mishahara na kutolipwa posho zao kwa wakati na kuchelewesha, Je, serikali inakabiliana vipi na changamoto hiyo ya maslahi kwa watumishi wa sekta hii muhimu?
Akijibu swali hilo, Bi. Kairuki alisema: “Serikali imeendelea najitihada zake za kuboresha mishahara yake hivyo kuboresha mishahara ya watumishi wake mwaka hadi mwaka ikiwemo ya wataalamu wa sekta ya afya kwa kuzingatia uwezo wa serikali wakulipa.”
Ameendelea kusema “Inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi na punde tathmini hiyo itakapokamilika serikali itapanga mishahara na motisha upya kwa watumishi wote wa umma wakiwemo wa sekta ya afya.
Ni kutokana na ukweli huu kati ya mwaka 2010-2011 hadi 2016 -2017 vianzia mishahara kwa kada za wauguzi zimeongezwa kutoka shilingi laki 6 na 14 elfu hadi kufikia shilingi 980 elfu kwa mwezi kwa wahitimu wa shahada na sh.425 elfu hadi sh. 680 elfu kwa mwezi kwa wahitimu wa stashahada, aidha shilingi 260 elfu hadi 432 elfu zitakuwa zikilipwa kama kianzio cha mshahara kwa wahitimu wa astashahada,” alifafanua.
Aliendelea kufafanua, “Kwa vianzia vya mishahara kwa kada za madaktari na maafisa tabibu katika kipindi hicho vimeongezwa kutoka shilingi 886 elfu na shilingi 800 hadi shilingi millioni 1.480 elfu kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425 elfu hadi shilingi 680 elfu, kwa wahitimu wa stashahada na mwisho ni shilingi 260 elfu hadi 432 elfu kwa wahitimu wa astashahada”.
Aidha Kairuki ametoa wito kwa kwa wataalam wa afya na watumishi wote kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia viapo na maadili ya kazi zao na kwamba serikali itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa kadri uwezo wake.