Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali inatarajia kuajiri watumishi wa idara ya afya ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi wenye vyeti feki.

Ummy Mwalimu ameyasema hayo jana wakati wa maadhimsho ya Siku ya Wauguzi Duniani ambapo kitaifa imefanyika katika hospitali ya St. Gasper, Itigi Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida.

Waziri Ummy amesema serikali inatambua mzigo mkubwa wa majukumu kutokana na uhaba wa wauguzi ambao umesababishwa na baadhi yao kuondolewa katika utumishi kwa kukosa vyeti halisi.

Pia ameagiza waajiri wa utumishi wa umma na hasa halmashauri zote nchini kupeleka maombi ya watumishi wa kada za afya ili wizara iweze kutangaza nafasi hizo zijazwe na watanzania wenye sifa.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Pulo Magesa amewataka wauguzi kuto muangusha waziri wao wa Afya kwa kuwa amekua mstari wa mbele kuhakikisha wauguzi na watumishi wote wa Sekta ya Afya Nchini wanafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha.

Magesa amesema serikali inaweka mazingira mazuri kwa kutenga bajeti ya kutosha ila ufanisi wake utaonekana endapo watumsihi wa sekta ya afya hasa wauguzi ambao ndio muhimili wa vituo vya huduma za afya mfano hospitali, zahanati na vituo vya afya watazingatia misingi ya uadilifu, upendo na weledi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema wauguzi wanaweza kupunguziwa mzigo wa kupata wagonjwa wengi hasa kwa magonjwa yanayozuilika endapo kutaanzishwa mfumo wa utoaji wa huduma za uuguzi kwa ngazi za kaya ambapo kila mwanafamilia atapewa elimu ya kuzuia baadhi ya magonjwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *