Jumla ya watuhumiwa 142 wamekamatwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya mkoani Mwanza katika kipindi cha Januari mosi hadi Februari 28, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alipokuwa akielezea hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Jeshi la Polisi katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Kamanda Msangi amesema dawa hizo zimekamatwa kutokana na jitihada za polisi kwa kushirikiana na wadau katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya mkoani Mwanza.
Amesema jumla ya watu 32 , wanaume 27 na wanawake 5 walikamatwa kwa kuwa na kilo 85 za mirungi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria. Kwa upande wa dawa za kulevya za viwandani, alisema kulikuwa na kesi 20 za heroine, ambapo kete 66 za heroine zenye uzito wa gramu 22 na pinchi 473 zilikamatwa.
Pia ameongeza kuwa kesi 70 zipo katika hatua mbalimbali za kiupelelezi, ambapo kati ya hizo, kesi 21 zinasubiri majibu kutoka kwa Mkemia wa Serikali, 39 zipo katika hatua ya upelelezi wa polisi na kesi 10 zimefungwa na polisi kutokana na kuwa na ushahidi dhaifu.
Amesema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa katika mkoa wa Mwanza kwa kuwa lina maadui wa ndani na nje na linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kulitokomeza.