Watu watano wamethibitishwa kufariki dunia na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa baada ya mshambuliaji kuvurumisha gari na kuwagonga watu katika daraja la Westminister jijini London.
Mshambuliaji huyo kisha alimdunga kisu afisa wa polisi lakini baadaye akauawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maeneo ya Bunge.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema shambulio hilo lilikuwa “la ukosefu wa maadili” na lilishambulia maadili makuu ya uhuru wa kufanya maamuzi, demokrasia na uhuru wa kujieleza.
Kaimu naibu kamishna wa polisi ambaye anasimamia kitengo cha kukabiliana na ugaidi katika Polisi wa Jiji Kuu, Mark Rowley, amesema anafikiria wanamfahamu mshambuliaji na kwamba huenda alihamasishwa na makundi ya kigaidi ya kimataifa yenye uhusiano na itikadi kali za Kiislamu.
Shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa 14.40 GMT pale mshambuliaji mmoja aliyekuwa na gari la rangi ya kijivu aina ya Hyundai i40 alipolivurumisha gari hadi eneo la kutumiwa na wanaotembea kwa miguu kwenye Daraja la West Minister, karibu na Majengo ya Bunge.
Baadaye, mshambuliaji huyo alikimbia, akiwa na kisu, hadi kwenye Bunge ambapo alikabiliwa na polisi.
Afisa wa polisi Palmer, ambaye hakuwa na silaha, alidungwa kisu na mshambuliaji huyo. Alifariki baadaye.