Watu zaidi ya 18 wamefariki dunia na wengine 50 wamejeruhiwa kutokana na kuibuka kimbunga kikali na hali mbaya ya hewa katika majimbo ya Georgia na Mississipi nchini Marekani.
Magavana wa majimbo hayo wametangaza hali ya tahadhari katika wilaya saba kusini na katikati mwa Georgia.
Bado kuna hatari ya kimbunga kupiga maeneo ya kusini mwa Florida, idara ya taifa ya hali ya hewa imesema.
Idara ya huduma za dharura ya Georgia imesema watu 14 walifariki katika wilaya za Cook, Brooks, Dougherty na Berrien katika jimbo la Georgia.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema amewasiliana na Gavana Deal na kumpa salamu za rambirambi kutokana na vifo vilivyotokea.
Kusini mwa Mississippi, watu wanne walifariki kutokana na kimbunga ambacho kilikuwa na upepo uliokuwa unavuma kwa kasi ya 218 km/h (136 mph).