Watu 12 wamethibitishwa kufa katika moto uliolitekeleza jengo la ghorofa 27 la Grenfell Tower jijini London nchini Uingereza.
Makundi kadhaa ya watu, wakiwemo watoto na wazee bado hawajulikani walipo katika jengo hilo la eneo la White City ambapo watu zaidi ya 79 walikimbizwa hospitali kwa matibabu.
Ghorofa hilo ambalo lina wakazi 600 lilikumbwa na taharuki kubwa ambapo watu walijaribu kila njia kujiokoa na moto huo ambao ulianza usiku wa manane ambapo ving’ora vya kuashiria moto katika jengo hilo havikufanya kazi.
Vyombo maalum vya kunyunyiza dawa ya kuzima moto navyo havikufanya kazi na njia maalum ya dharura ya kupita wakati wa majanga ya moto, ilikuwa imezibwa.
Hata hivyo, moto huo hatimaye ulifanikiwa kuzimwa jana na vikosi vya zimamoto na kuliacha jengo likiwa limeungua vibaya.