Serikali mkoani Dodoma inatarajia kufanya operesheni ya kuwaondoa watoto wa mitaani, ambao wamekuwa kero kwa wapita njia na wateja wanaokula hotelini, ambao huwanyang’anya chakula na hata vinywaji wateja.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme amesema watawaondoa watoto hao kutokana na kuwa hatari kwa maisha ya watu wengine.
Mndeme amesema watoto hao wamekuwa wakikaa makundi na kuvuta dawa za kulevya aina ya gundi na wamekuwa wakiingia kwenye hoteli na kunyang’anya wateja vyakula na hata vinywaji.
Amesema watoto hao wamekuwa wakikaa kwenye makundi na kuwa tishio kwa wapita njia hasa nyakati za jioni kutokana na kujihusisha na uhalifu.
Pia alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watoto hao kuingia hotelini na kuwanyang’anya wateja chakula na vinywaji kisha kukimbia, jambo ambalo halileti picha nzuri na vitendo hivyo vinatakiwa kudhibitiwa.
Mkuu wa Wilaya huyo ameongeza kwa kusema watachukua hatua hiyo kwa umakini ili watoto watakaoondolewa wasirudi tena mitaani, kwani inaonesha miaka ya nyuma lilifanyika lakini baada ya muda watoto hao walirudi tena mitaani.