Watanzania wametakiwa kutumia korosho zinazozalishwa nchini kwani bidhaa hiyo ni muhimu katika kulinda afya zao.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha (pichani) alisema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya bidhaa ya korosho katika Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa (DITF), yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Ole Nasha alitaja matumizi ya korosho kuwa ni kupunguza uzito uliopitiliza, magonjwa ya shinikizo la damu, kuboresha mfumo wa ubongo, kuimarisha afya na kuliingizia taifa fedha za kigeni.
“Iwapo Watanzania wataelimishwa ipasavyo na kuona umuhimu wa matumizi ya bidhaa hiyo kuna nafasi kubwa katika kukuza soko la ndani na kuleta tija katika afya zao,”alisema.
Alisema serikali imejipanga kuhakikisha mbolea ya zao hilo inakuwa na bei elekezi ili kupunguza gharama ya kilimo hicho na kuongeza kuwa pia watahakikisha wanatoa tani 18000 kwa ajili ya kuwafikia wakulima wadogo.